Saturday, May 4, 2013

MWALIMU WA MADRASAT ALIYEMLAWITI MWANAFUNZI AFUNGWA JELA MIAKA 15 HUKO ZANZIBAR

BAADA ya mahakama ya mkoa Vuga kumwachilia huru mwalimu wa madrasat Qadiria iliyopo Amani wilaya ya Mjini Unguja, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumlawiti mwanafunzi wake wa kiume wa miaka 11, hatimae mahakama kuu ya Zanzibar imemfunga jela miaka 15.

 Uamuzi huo wa mahakama umekuja kufuatia rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),  kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya Mkoa.

 Pamoja na adhabu hiyo, mahakama imemtaka kulipa fidia ya shilingi 500,000 dhidi ya mtoto huyo mdogo aliyemfanyia kitendo hicho.

 Mahakama hiyo, chini ya Jaji Abdulhakim Ameir Issa imelazimika kutoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na sababu za rufaa zilizowasilishwa na DPP, ambazo zilidai kuwa mahakama ya mkoa Vuga imekosea kisheria katika utoaji wa hukumu.

Hivyo, baada ya kusikiliza kwa kina hoja za pande mbili hizo juu ya rufaa hiyo pamoja na kuangalia vielelezo vya ushahidi vilivyotolewa katika mahakama ya mkoa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, Jaji Abdulhakim alisema mahakama ya mkoa ilikosea kisheria katika utoaji wa hukumu.

Jaji huyo alilazimika kutengua uamuzi wa mahakama ya Mkoa na kumtia hatiani Ustadh huyo dhidi ya shitaka hilo la kumuingilia mtoto wa kiume kinyume cha maumbile lililokuwa likimkabili.

 "Mahakama inatengua uamuzi wa mahakama ya mkoa kwa sababu ilikosea kisheria katika utoaji wake wa hukumu, hivyo mahakama hii inaamuru kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 15, haki ya rufaa ipo wazi kwa upande ambao haukuridhika na uamuzi huu," alisema Jaji Abdulhakim.

 Sambamba na adhabu hiyo, Jaji Abdulhakim alimtaka Ustadhi huyo kulipa fidia ya shilingi 500,000 kwa mtoto huyo aliyemfanyia kitendo hicho.

 Katika rufaa hiyo upande wa DPP uliongozwa na Mwanasheria wa serikali Maulid Ame Mohammed, kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.

 Ustadh Hamadi Bakari Mohammed, miaka 48, alikuwa akikabiliwa na kesi ya kumuingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi wake wa kiume wa miaka 11, kesi ambayo ilikua chini ya hakimu Makame Mshamba Simgeni wa mahakama ya mkoa Vuga.

 Kesi hiyo ilifunguliwa kwa mara ya kwanza Julai 7, 2011 ambapo alikana shitaka hilo baada ya kusomewa na Mwanasheria wa serikali Juma Msafiri Karibona, kutoka ofisi ya DPP.

 Pamoja na kukana huko, upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi sita mahakamani hapo, lakini walishindwa kuthibitisha kosa hilo kwa mujibu wa hakimu Makame Mshamba Simgeni kwa maelezo kuwa ushahidi wao ulijaa shaka ya maana.

 Hivyo, Januari 18 mwaka jana, mahakama hiyo ya mkoa ilimuona hana hatia dhidi ya kesi hiyo na kumuachilia huru chini ya kifungu cha 219 cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

 Wakati mahakama hiyo ya mkoa ikitoa hukumu hiyo, mshitakiwa huyo alikuwa nje kwa dhamana ya fedha taslimu shilingi 150,000 kwa wadhamini wawili pamoja bondi ya shilingi 300,000 kwa upande wake.

 Kwa upande wa mahakama kuu, Jaji Abdulhakim alimwachilia kwa dhamana ya wadhamini wawili wenye vitambulisho, mmoja kwa fedha taslimu shilingi 1,000,000 na mwengine kwa bondi ya shilingi 300,000.

 Ilifahamishwa, kinyume na kifungu cha 132 (1) sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, Januari 13, 2011 majira ya saa 2:30 za asubuhi, huko Amani alimuingilia kinyume cha maumbile mtoto huyo wa kiume (jina tunamuhifadhi).

 Pamoja na adhabu hiyo aliyopewa na mahakama, Ustadh Hamad aliwahi kukaa rumande kwa muda wa siku 16, baada ya upande wa mashitaka kupinga kupatiwa dhamana kwa mara ya kwanza alipofikishwa mahakama ya mkoa, kwa madai anaweza kuingilia kati upelelezi ambao kwa wakati huo ulikuwa bado haujakamilika.

No comments:

Post a Comment